Mtunzi: Odhiambo Danyell
Ni bayana kwamba wenyeji wa Nairobi na vitongoji vyake wana kila
sababu ya kutabasamu baada ya tangazo la kufungwa kwa soko maarufu la
nyama kwa jina Burma. Hatua hii imechochewa na tabia ya wafanyi
biashara kukaidi kutii sheria za wakaguzi wa afya.
Kabla ya kungamua hatari inayowakodolea macho walamba minofu katika
soko hilo ni heri nikufafanulie taswira halisi angalau ufahamu
chimbuko la hatua hii. Punde tuu unapofika katika lango kuu la soko
hilo utakaribishwa na harufu mbaya inayoninginia hewani.
Kando na hayo, utashuhudia jaa kubwa la taka la kusheheni pembe za
wanyama, makombo ya minofu pamoja na maji taka iliyozagaa kila sehemu.
Hatimaye, utawaona chokora wakibishana na mbwa ambao hukukwangura jaa
hilo wakitafuta pato lao.
Kuingia ndani, utapishana na wafanyi biashara wa nyama waliovalia
ovaroli chafu za kutona damu wakibeba bidhaa hiyo kiholela huku
wakivuka mitaro iliyosakamwa na maji taka iliyoganda wakati
wakisindikizwa na vikosi vya nzi.
Aidha, kwenye maduka na hoteli , hutakosa kujionea jeshi kubwa la nzi
ambao wameteka nyara kila sehemu hata kuwalazimisha wenyeji kurusha
rusha mikono wakati wakiendelea kufurahia mapishi rojorojo ambayo
huandaliwa kwenye hoteli hizo za Burma.
Tushamhoji mgonjwa na sasa hatuna budi kugeukia daktari angaa tupate
tiba kwa hali hii mbaya kwa vile ni wazi, tusipojenga ufa tutajenga
ukuta. Hivyo, wakati tukiwakemea wafanyibiahsra wa Burma na kukumbatia
hatua ya kufunga soko hilo ni muhimu mikakati kabambe iwekwe ili
kuepusha wenyeji wa soko hilo na mikurupuko ya magonjwa.
Hayo ni tisa, kumi ni kwamba ili kupata suluhisho la kudumu soko hilo
lafaa kubomolewa na hatimaye kujengwa upya huku wakizingatia miundo
msingi za kuimarisha usafi. Aidha, sheria za baraza la jiji pamoja na
zile za wizara husika zinapaswa kukazwa. Mwisho, wenyeji wanapaswa
kufanyiwa hamasisho kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi na hatari ya
kuendelea kufanya kazi zao katika mazingira hayo.
Comments