Skip to main content

OPERATION TUTETEE WANAUME!!!

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL
SEHEMU YA KWANZA:

Mzee Matendechere alionekana kuokotwa na usingizi mwepesi wakati akiuguza majeraha ya panga hospitalini. Kisa na maana, adabu ilimhama mkewe hata akaamua kuchukua sheria mkononi na kumpa mumewe kichapo cha mbwa kabla ya kutorokea kusichojulikana.

Kichwa chake kilibanwa kwa kilemba cheupe chenye matone ya damu. Isitoshe, Kwenye shavu la kushoto, palidhihirika jeraha bichi lenye kushonwa kwa uzi. Cha kusikitisha zaidi, Pembezoni mwa kitanda, wangeonekana wapiga picha kutoka vyumba vya habari waking’ang’ana kuchukua picha za kuvutia watazamaji.
picha kwa hisani ya http://medievalminds.com


Maskini Matendechere alizidiwa na usingizi hata akabakia kukoroma huku akifungua mdomo mithili ya mamba mwenye njaa. “Wow! This seems to be the best shot, I,m loving this” alisikika akisema mmoja wa wapigaji picha tuliyeshuku ni wa asili ya kimarekani. Kweli, vita vya panzi furaha ya kunguru.

Wakati haya yakijiri, ndoto ya matukio yaliyotendeka kabla ya masaibu haya kumpata Matendechere yalivamia mawazo yake. Akilini, alijaribu kukusanya picha hizo bila ya kitendawili cha asili ya maumivu yake kuteguka.

Midundo mizito ya rumba ilizidi kufagilia katika mkahawa maarufu wa ‘tamasha’ katika barabara ya tugawe umaskini. Kama kuchokoza wenye kuneng’ua viuno kwenye sakafu, Deejay Manyoya aliwachilia kibao maarufu ‘I,m not sober’ cha bendi maarufu ya Jamnazi Afrika. Kauli hii ilisindikizwa na vifijo na nderemo. ungedhani ni karamu ya kukaribisha kurudi kwa Yesu. Haya yakijiri, baadhi ya wenyeji walizidi kumimina chupa za mvinyo macho wakibandika kwenye runinga.

Wakati huu wote, Mzee Matendechere alikuwa amechokorwa kichwa na mizimwi ya mvinyo kiasi ya kwamba aliridhia kutafuta starehe kwenye kochi kando ya ‘counter’.

Ukitizama kushoto, ungeona kundi la makahaba ambao walikuwa wamejikwatua kwatu kwatu wakianika mitego yao tayari kunasa wateja. Mwingine alivalia ‘tumbo cut’ ya kubana kifua yenye maandishi “usiseme maziwa, sema ngombe”. Isitoshe, alivalia sketi fupi iliyofichua mapaja yake yenye madoadoa utadhani ni wa jamii ya chui au fisi.

Wakati viumbe hawa wakisasambua mapaja yao kwa wapita njia, Mzee Matendechere alibakia kuvuta mabaki ya sigara yaliyoangushwa na wateja sakafuni. Baba mtu alizubaishwa na vimulimuli vya taa ya ‘disco light’ akakaribisha moshi ndani ya mapafu kabla ya kuwachilia wingu kubwa hewani.

“Mzee! Inuka uende nyumbani. Tuko karibu kufunga na hatutaki ukamatwe na polisi” wahudumu pale kwenye mkahawa walimrai. “Kwani huyo Mututho anadhani ni nani atupimie starehe na pesa tunakunywa ni zetu? Leta kingfisher mbili hapo.” alisikika Matendechere akizusha kwa ujeuri huku akilaani mbunge aliyebuni sheria inayopima masaa ya kunywa pombe.

Wakati Matendechere akizizana na wale wahudumu , ghafla fikra zake zilivutiwa na maandishi FulanI ukutani. “Customers have a right to stay and to pay”. “Haya ndiyo madhara ya kususia masomo mapema. Can you please read the bold writings on the wall?” Mzee Matendechere aliwakabili huku akionekana kuzidiwa na kichefuchefu.

Kwa dakika zile chache, baba mtu alijiona jogoo wa kukomaa. kuwika kwake kuliwatisha wahudumu. Kwenye lango kuu la mkahawa, tayari wateja wengine wangeonekana wakiondoka wameshikana taratibu kumaanisha walikuwa wameona dalili ya . Kadri masaa yalivyoyoma ndivyo shughuli zilipungua pale hata mziki ikazimwa na stima kuzimwa.

“Ala! Mzee, hii ni siku ya pili tunakutoa hapa kwa nguvu. Kwani huna familia? Enda nyumbani tunafunga.” Askari aliyeshika doria langoni alimzomea Matendechere.

Baadaye, baba mtu aliona amezidiwa maarifa hata akajikusanya na kutembea taratibu akieleka nyumbani. Barabarani, hungempita bila ya kumtambua kutokana na kuimba kwake. “I,m not sober Odiero, I,m not sober……..i,m not sober because I,ve taken guiness.”hivyo ndivyo hali ilikuwa.

Ilibakia kona moja tuu kabla ya kuwasili kwenye maskani yake katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani pale Soweto. Pale, aliteleza na kuanguka kwenye mtaro ya maji taka. “Auuuwi!.... Auuuwi! Mama Wanjiru bwana yako ameingia kwenye mtaro. Njoo tumsaidie” mama mmoja msamaria mwema alipaza sauti na kuvutia umati.

SHUKRAN!!!!
Endelea kufuatilia hadithi hii kujua kinachojiri!!!!!........

Comments

Popular posts from this blog

MAZINGAOMBWE YA SAA

Na Danyell Odhiambo Nimejirusha kwenye kiti kilegevu cha msonobari nikifikiria jinsi hali ya maisha nchini Kenya inavyozidi kupaa kila uchao. Mbele yangu, pametulia redio, kando pamesimama kikombe cha kahawa chungu na juu pananinginia saa ya ukuta. Ghafla, fikra zangu zinatekwa nyara na saa iliyozubaa ukutani. Nikiangazaangaza, naona imetimia usiku mkuu. Hii ni kumaanisha, mishale yote ya saa imekutana kifuani pa namba kumi na mbili. Ukipiga hesabu kwa makini, utakubalina nami kwamba tukio kama hili hujirudia mara mia tatu sitini na tano kila mwaka. Ukumbuke, kisa hiki pia huashiria kuzaliwa kwa siku mpya. Hata ingawa mishale hizi zimedhibitisha ushirikiano ni kiungo muhimu katika katika kikundi, taswira fulani inaibuka nikiangalia mishale hizo. Taswira yenyewe yahusu tabia mbovu ya wabunge kukaidi shinikizo za kuwataka kulipa malimbikizi yao ya kodi. Nikipamabanua kitendawili hiki, itakubali kwamba jamii imejigawanya kupitia mishale hizi tatu za saa. Mahuluku taabu nawafa...

MAPENZI KIZUNGU ZUNGU

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL Mawimbi makali baharini yalikimbizana na hatimaye kusukuma maji hadi ufukweni. Pembeni, Bahati alionekana ameshika kijiti kirefu mkononi akijaribu kuchora umbo la moyo wa mapenzi kwenye changarawe mbichi huku maji ya bahari yakifuta. Angani, ndege aina ya korongo na mbayu wayu wangeonekana wakicheza cheza huku tufani kali zikifanya matawi ya minazi ufuoni kupukutika. Nikijistiri juu ya roshani(balcony) katika hoteli ambayo tulikuwa tumekodisha nilisalia kula kwa macho. Nilibakia kinywa wazi kuona madhari ya kutamanisha jinsi jua ilizama upeoni na kufanya maji ya bahari kupiga rangi ya manjano. mawazoni, nilitawaliwa na picha za harusi yetu jana yake katika ukumbi wa pataneni . Hatua chache niliona suti yangu ambayo ilikuwa ingali sakafuni baada ya usiku yenye sarakasi si kidogo. Ajabu, marashi yenye uhai aliyopiga Bahati ilikuwa bado imesakama pua yangu.Waliosema harusi ni kilele cha mapenzi hawakukosea hata kidogo. “Honey…………Rashidy! Rashidy!” Kwa...

SIRI ZA CHUO KIKUU CHA DAYSTAR

Njoo unisome kwa makini S.L.P 927 MACHO PLAZA Kwa wewe unayenisoma, Habari za utokako? Naona unahema kweli ukitaka kujua yaliyojiri hivi leo kwenye barua hii. Hee! By the way, ikiwa wataka tuelewane naomba uwache kuniangalia kwa hizo macho za kushiba chuki na dharau. Kabla nikuendelezee udaku! Tafadhali wacha kuangalia kando kando ukinisoma. Unawafanya wapita njia wanadhani tunawasengenya humu. By the way, usha ambiwa na yeyote hivi leo kwamba watamanisha? Ooooooooooooh! Nisamehe. I mean.... you are fearfully and wonderfully made. Sitaongeza wala sitapunguza. Niwie radhi siwes kutranslate, please! Mwelezee.. aliye kando yako aje akusaidie. Kabla nikupatie udaku, natamani niulize swali moja tuu. Nihakikishie kwamba hutanuna! Naogopa lakini heri niulize tuu atleast tusafiane nia. Hivi mbona una blush sana? Kama nimekubamba si uniambie tuu ama uwaite wanafunzi wenzako waje wasome uhondo. Matawi ya miti naona inapukutika kutokana na upepo mkali unaofagilia kutoka milima ya l...