Skip to main content

SIRI ZA “JAM” JIJINI NAIROBI; TOLEO LA PILI

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL

Jinsi basi lilivyozidi kufukuzia kuelekea mzunguko wa Nyayo stadium, ndivyo ilizidi kuwachilia moshi ya mpingo iliyosokota angani kabla ya kutawanyika. Pale pia, tulimpata polisi wa trafiki mwanamke aliyefungia mshipi wa longi yake kwenye kifua. Amini usiamini, kwa ishara ya mkono alielekeza mkondo wa gari kama jinsi upepo huele...keza bendera.

Pale tulis...imama kwa dakika chache kabla ya msongamano kufunguliwa. Cha kuvutia tamaa ya macho yangu ilikuwa ‘tuk tuk’ fulani ambayo ilipenya penya kati kati ya magari huku ikipiga kelele kama mashine ya kusaga mahindi. Wenzangu wanaiita kule bara POSHOMILL. “We! Boss, ondoa hiyo kabati kwenye barabara” alisikika akishambuliwa na mmoja wa madereva wa matatu.



Wanasema muungwana hununa moyoni na wala siyo mashavuni na kwa hivyo Yule dereva wa ‘tuk tuk’ akaridhia kumjibu kwa kimya. Kando na tukio hili, kuna jambo lililotendeka ambalo liliwacha mbavu za kila mtu zikiuma.

Niseme nisiseme! Aaaah! Heri niseme angalau na wewe uonje uhondo. Hayaa! Kuna huyu omba omba aliyejifanya kuakalia miguu yake akijidai kilema. Isitoshe,uso wake ulijichora picha ya masumbuko bin mateso hata wapita njia wakamsikitikia na kumrushia sarafu kwenye kijisahani chake.

Ajabu! Kuna hili trela la magurudumu kumi na kadhaa la kubeba simiti lililopita karibu na hapo kabla ya kusimamishwa na yule polisi mwanamke. Ghafla! Kilichofuata kilikuwa ni mlipuko mkubwa ajabu uliobadilisha hali pale kuwa ya mguu niponye. Kumbe ni magurudumu yake mawili yalipasuka na kuibua sauti sawia nay a bomu.

Kilema huyoo! Alitia pato lake mfukoni kabla ya kukata kona akitafuta usalama wake. Ama kwa hakika, kisa hiki kiliwacha wengi mdomo wazi hasaa wasafiri waliokuwa wanasubiri matatu hapo karibu. “lo! Kajifanya kilema kumbe ni bingwa wa riadha?” nilijisemeza huku nikifungia kicheko baada ya mbavu kuanza kuuma.

Safari iliendelea, basi ikajikaza kupanda milima na kutereka mabonde hata tukafikia njia panda ya kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa JomoKenyatta. Katika maisha yangu, nimetamani vitu viwili tuu; kwenda mbinguni na kuabiri ndege.

Kwa umbali, ningeona ndege kadhaa zimeegeshwa nje ya mabohari zikipakiwa mizigo. Nikiwa nimezama katika dimbwi la mawazo,, nilishangaa kuwasikia wanaume fulani kwenye kiti kando yangu wakinong’ona. “Masalale! toto lenyewe fupi tena limetimia” huo ndio usemi uliozindua mafikira yangu hata nikarusha macho nje ya dirisha la basi kujua yaliyokuwa yanajiri.

Dododooooooo! Pale kando ya basi palifukuzia gari aina ya BMW X6 almaarufu ‘Be My Wife’. Ndani aliketi dereva mwanadada wa kuvalia minisketi ya kufichua magoti. Mdomoni alishikilia peremende ya ‘Pinpop’ huku picha yake akinakshiwa kwa vipuli vilivyong,aa si kidogo. Ya mrembo, tuyawache, sitaki tukeshe hapo. Najua wenzangu waume watapoteza makini ya hadithi hii. Heri tushughulikie ya BMW.

Yaitwa BMW, nyumbani kwao alikozaliwa ni katika nchi ya ujerumani kule bara uropa. Ulafi wa petrol ni lita kumi na mbili kwa kila kilomita mia moja. Ukisawazisha na maumbile ya mawanadada, gari hili lina kifua cha wastani, makalio maridhawa na mgurumo wa kumtoa nyoka pangoni. Mashallah! kidosho wa kuteka nyara fikra za wengi.

Taratibu, gari hilo liliruka kwenye tuta za kupunguza kasi na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye lango kuu la uwanja wa ndege. Asiye na mwana aelekee jiwe, kila mmoja aligeuza fikra na kurudi katika shughuli za kawaida.

“miwa ni kumi! miwa ni kumi! ………miwa ni kumi!” hiyo ndiyo taarifa iliyotukaribishatulipowasili mji wa mlolongo. Huku haya yakijiri, dereva naye alikazana kupisha trela ambazo zilikuwa zinaingia katika stesheni ya kupima uzani. Zingine zilibaki kuegeshwa ovyo ovyo kando ya barabara na hivyo kufanya eneo hilo kuwa hatari sana.

Hatua chache, tungesikia midundo ya aina ya KATITO ikipenyeza kutoka kilabu moja ya burudani karibu na barabara. Ningewaona wenye mihela wakimimina machupa ya mvinyo kwenye roshani (balcony) ya hoteli hiyo huku mmoja akicheka kiasi cha kuinua mguu juu. ndo starehe za nyani kukalia mkia na kulalia masikio. haahahahaaha!

“Jumatatu na mtu tayari anaburudika na mvinyo mapema hivi?” aliuliza mmoja wetu kwenye basi. “Dunia ni yao, ukipewa pia utatekwa nyara na uraibu fulani” alijibiwa bila kusita.

Basi ya kisasa aina ya OXYGEN ama Mordern Coast ilipita kwa kasi na kuokota mawazo ya kila mtu. Kila mmoja, alikuwa na sifa spesheli aliyolimbikizia basi hilo. “Itakuaje mkifanikiwa kupanda ndege?” heri ningepewa nafasi ya kuwauliza swali hilo hadharani. Ukistaajabu ya musa utaona ya firauni.

Comments

Popular posts from this blog

MAZINGAOMBWE YA SAA

Na Danyell Odhiambo Nimejirusha kwenye kiti kilegevu cha msonobari nikifikiria jinsi hali ya maisha nchini Kenya inavyozidi kupaa kila uchao. Mbele yangu, pametulia redio, kando pamesimama kikombe cha kahawa chungu na juu pananinginia saa ya ukuta. Ghafla, fikra zangu zinatekwa nyara na saa iliyozubaa ukutani. Nikiangazaangaza, naona imetimia usiku mkuu. Hii ni kumaanisha, mishale yote ya saa imekutana kifuani pa namba kumi na mbili. Ukipiga hesabu kwa makini, utakubalina nami kwamba tukio kama hili hujirudia mara mia tatu sitini na tano kila mwaka. Ukumbuke, kisa hiki pia huashiria kuzaliwa kwa siku mpya. Hata ingawa mishale hizi zimedhibitisha ushirikiano ni kiungo muhimu katika katika kikundi, taswira fulani inaibuka nikiangalia mishale hizo. Taswira yenyewe yahusu tabia mbovu ya wabunge kukaidi shinikizo za kuwataka kulipa malimbikizi yao ya kodi. Nikipamabanua kitendawili hiki, itakubali kwamba jamii imejigawanya kupitia mishale hizi tatu za saa. Mahuluku taabu nawafa...

MAPENZI KIZUNGU ZUNGU

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL Mawimbi makali baharini yalikimbizana na hatimaye kusukuma maji hadi ufukweni. Pembeni, Bahati alionekana ameshika kijiti kirefu mkononi akijaribu kuchora umbo la moyo wa mapenzi kwenye changarawe mbichi huku maji ya bahari yakifuta. Angani, ndege aina ya korongo na mbayu wayu wangeonekana wakicheza cheza huku tufani kali zikifanya matawi ya minazi ufuoni kupukutika. Nikijistiri juu ya roshani(balcony) katika hoteli ambayo tulikuwa tumekodisha nilisalia kula kwa macho. Nilibakia kinywa wazi kuona madhari ya kutamanisha jinsi jua ilizama upeoni na kufanya maji ya bahari kupiga rangi ya manjano. mawazoni, nilitawaliwa na picha za harusi yetu jana yake katika ukumbi wa pataneni . Hatua chache niliona suti yangu ambayo ilikuwa ingali sakafuni baada ya usiku yenye sarakasi si kidogo. Ajabu, marashi yenye uhai aliyopiga Bahati ilikuwa bado imesakama pua yangu.Waliosema harusi ni kilele cha mapenzi hawakukosea hata kidogo. “Honey…………Rashidy! Rashidy!” Kwa...