MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL
CHUO KIKUU CHA DAYSTAR
NAIROBI
Magurudumu ya matatu yalikimbizana kuelekea kwenye lango kuu la ziwa Baringo. Nyuma yetu barabara ilikuwa safi japo kwa vumbi nyepesi pamoja na moshi ambayo ilionekana kutuandama kabla ya kusokota angani.
Pembeni mwa lango hilo, palisimama wima kibao “Welcome to Lake Baringo” hii ikawa ni ridhisho tosha kwamba makaribisho kabambe yalikuwa yatungoja. Kama ada, tuliegesha gari mbele ya kizuizi cha baraza la jiji. yaliyofuata, yakawa ni kuhesabiwa kisha kulipia kiingilio. “Karibuni na mjienjoy kabisa” askari kwenye lango alitueleza.
Baadaye, kizuizi kiliinuliwa kuashiria tulikuwa huru kuvinjari kila kona ya ziwa ambalo nilikuwa nimesikia tuu kupitia uvumi wa marafiki pamoja na maarifa ya vitabu za jiografia.
Kuonekana kwa ziwa upeoni kuliwafanya hata waliokuwa wanasinzia kupata sababu ya kuchangamka. “Lake Baringo here we come!” kidosho aliyekuwa kando yangu alisema wakati akingangana kupiga picha kutumia simu yake ya rununu. Ajabu zaidi, alikosa kutulia kiasi ya kutoa shingo dirishani utadhani kaona mbinguni.
Bila kusita, dereva naye alirukia kiti chake , akajifunga mshipi , kubadilisha giya. ufunguo wa gari uliingia mahala pake na Vrrrrrrmm! Vrrrrrrmm! Vrrrrrrmm! tukaondoka.
Moja kwa moja, tulifululiza hadi kwenye maduka viungani mwa ziwa hilo angalau kushughulikia shinikizo za minyoo ambao tayari walikuwa wanatishia kuandamna tumboni..
Wanasema, ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni. Punde tuu tuliponunua kreti ya soda na mandazi ndipo tulishuhudia maajabu.
Kwanza, kunguru wawili kumbe walikuwa wamepata mwanya kwenye dirisha wazi na wakabaki kujipakulia chakula kidogo iliyokuwa kwenye gari. Sitasema walikuwa wanakula popcoon.
“Kaisari amekuja kuchukua kilicho chake” kijana mmoja alitania na kuibua kicheko si kidogo.
Isitoshe, Kama vile siafu wanavyomvamia chakula chao, jeshi lile la watoto lingeonekana likitukaribia pasi na sisi kujua walikuwa wanapanga nini dhidi yetu. “Uncle nipatie shilingi kumi” alisikika mmoja akisema.
Akivaliwa na sura ya ukarimu, dereva aliingia mfukoni, akachomoa jani la shilingi hamsini na kumpa mmoja wao akidhani hii ingetunasua kutoka mtego huo. “Hawa ni masonko!” alisikika mmoja wao akimnongonezea mwenzake. Gahfla, wimbo ulibadilika na kuwa “Na mimi jee uncle?”
Kumbe alikuwa kachokoza nyuki.utngedhani amepiga mbiu ya mgambo kwani umati ule ulijikusanya kama kutaka kumparamia dereva.wanasema lisilo budi hutendwa na kwa hivyo, ikabaki tumevalia sura za ukali ndipo wakatawanyika.
Baadaye, tulielekea kwenye maegesho ya gari na likafuatia sala ya kulinda ziara letu. mmoja baada ya mwingine, bila kusita, tuliambua nyayo taratibu hadi kwenye ufuo wa ziwa Baringo. Njiani, hatungeepuka kuteleza kwenye chochoro za mawe ambazo zilichongeka kutokana na kazi ya miaka nyingi. amini usiamini, mawe zilichongeka utadhani panga.
Kushoto, tungewaona watalii wakifurahia kuzungushwa kwa kasi na motaboti ya samawati ambayo ncha yake ilipasua maji kama wembe. kando kandowalizingirwa na wavuvi kwenye madau yao madogo wakiendelea na tafuta tafuta zao.
“Uncle si ukule kasamaki choma” aliniuliza mmoja wa wachuuzi. “Pesa ngapi?” nikauliza. “mia tatu tuu kwa kipande kimoja” alijibu huku akisongesha sinia karibu na pua langu.labda aliamini hii ni mtego tosha kwa kuchokoza hamu yangu. nikielekeza mkono mfukoni ndipo nilikucha zake za kustiri uchafu hata hamu ikanitoka.
“Tupande motaboti kwanza halafu tuatarudi kula samaki”binti fulani alitoa wazo la kuninusuru na kukatiza biashara yetu. Hii ilimfanya mchuuzi Yule kuudhika ungedhani kaumwa na nyuki.
Kwa dakika kadhaa mawazo yangu yaliibiwa na mwanadada mmoja ambaye alifanya moyo kunideka ovyo ovyo. Kaskazini alivalia "tumbo cut" ama kata tumbo yenye maandishi "look but dont touch", kusini alikuwa amebana kumakalio yake ya kushiba ndani ya minisketi fupi iliyofichua mapaja yake. Mengine sitasema ukitaka kujua zaidi, njoo ntakuonyeshe picha.
Wakati tukisubiri kiongozi wetu kuelewana kuhusu nauli ya kusafiri motaboti tuliridhia kuketi chini ya kitalu cha miti. hii ni kutokana na jua kali iliyokuwa inangaa utadhani inashirikiana na watoto wake. Kwa mtu mweusi kama mimi niliogopa kunuka moshi.Wenzangu walichirizikwa na jasho njia mbili mbili mashavuni utadhani mvua kubwa yanyesha katika msitu wa nywele utosini.
“Kaka hebu njoo” sauti dhabiti na yenye ukaidi iliniita kutoka nyuma.mtu hakatai wito bali aitwalo. “Enhe nikusaidiaje?”niliitika na kusogelea alipokuwa.
Jamaa huyo alinitisha kwa jinsi alivalia miwani pamoja na rasta zilizochakaa. Alinikumbusha jambazi fulani kijijini aliyeogopewa kwa ustadi wake wa kuiba mayai ya kuku pamoja na vifaranga. ikiwa umeona majarida ya sokwe mtu basi utafahamu kile ninachozungumzia.
“Hapo mmeketi ni ufuo wa kibinafsi. Kuweka mkutano kwenye jiwe hilo litawagharimu shilingi mia kila mmoja ” aliongea huku akinyosha mkono kama wa kuataka vita.
“Hatulipi na hatulipi! Mmemetuzoea sana” kidosho aliyekuwa anategea sikio mazungumzo yetu alitukatiza na hivyo kuchemsha hasira ya 'rastaman'.
"Hey! Mashaka kuwa mpole hapa si kwetu na hatutaki kuzua sokomoko ugenini." niliingilia kati angalau kutuliza temprecha za 'sokwe' yule.
"Una bahati sana niliamka kwa maombi, stupid! who do you think you are?" Rasta man alimjibu.
Kama wakristo watiifu, baadaye tuliweza kumrai 'rastaman' kutupunguzia bei hata baadaye akaridhia kukubali kuchukua shilingi hamsini. Wakati huo wote tukibishana, jeshi la watoto ombaomba lilikuwa limetuzingira.
“Mwenye motaboti amesema kila mmoja atatoa shilingi mia tatu ili kuabiri boti lake hadi kisiwani" alitangaza kiongozi. wachache walikubali kulipa na wakandamana naye kuabiri boti.
Tukikadiria kwa macho, kisiwa kile kilikuwa takriban mita mia tano hivi kutoka tulipokuwa. “Heri nikule samaki. Hiyo ni nauli ya kutoka Nairobi hadi mji wa Eldoret” kijana mmoja mbishani alidakia na kuibua kicheko.
Usemi huo uliwaleta wachuuzi wa samaki hata karibu na hiyo ikachochea wale waoga wa kusafiri majini kununua samaki ambayo tulikula shingo upande. kinaya ni kwamba, wachuuzi hawa walifuatwa na mbwa waliokuwa wamekonda kiasi ya kwamba mbavu zao zingehesabika.
“Mbona mbwa wa huku wamekonda hivi ilhali wanaishi penye soko kubwa la samaki?” dada mmoja aliuliza. Mmoja wa wachuuzi wale alicheka huku akijibu kwamba mbwa ana ustadi wa kuogelea na kwa hivyo haoni maana ya mbwa kulala njaa ilhali anaweza kujitafutia samaki baharini. "Sisemi kitu" nilisema kimoyomoyo huku nikisonya.
Minyoo tumboni walikuwa wameanza maandamano na kwa hivyo tulianza kutoa vyakula mbalimbali tulivyokuwa tumebeba. Ushawahi kuangaliwa na macho ambayo yanakumulika mpaka moyoni?
Hivyo ndivyo hali ilikuwa pale. Kwa kila tonge ulichomeza watoto wale walikuangalia kwa macho ya huruma. kama ambao wanakulaani. ukidhani nakudanganya, chupa yangu ya soda iliteleza na kumwagika. Ghafla, mbwa mmoja kijivu wa kufanana na jamii ya fisi alinikaribia kuanza kulamba jiwe palipomwagika soda. Kweli baa la njaa ni janga la kitaifa.
Baadaye tulihama pale na kuelekea ufuoni palipokuwa na mamba ambao walikuwa wamezoeana na binadamu. Tulipata kundi la vijana fulani chipukizi wakiwalisha matumbo. Walituamkua kabla ya kutukaribisha kupiga picha karibu na mamba.
Kwa vila nazijua hatari za mzee mamba nilisalia kuzitizama kwa mbali huku milio ya ndege aina ya korongo na kunguru ikitawala angani. Wenzangu walifurahia wakati kijana mmoja alipopanua mdomo wa mamba akijaribu kuwadhihirishia maajabu kwamba mamba hana ulimi.
Sarakasi ilipofikia kikomo kundi la vijana lilituzingira na kutushrutisha kutoa shilingi mia moja. Hii ikiwa ni gharama ya kupiga picha pamoja na kupewa mafunzo. Baadhi walikubali kulipa huku wengine kama sisi tuliotizamna kwa mbali tukidinda.
“lazima mtulipe! Kwani mnadhani tunakula nini hapa?” kijana mmoja mtukutu akaanzisha mabishano akielekea tulipokuwa tumeketi.
Usalama wetu ulikuwa haupo tena na kwa hivyo kidosho yule akasalia kubadilisha maneno na wao. “ Mnafaa kufunzwa jinsi ya kuwakaribisha wageni kwani ni wazi nyinyi wenyewe mna angamiza utalii ziwani humu” aliwaeleza.
“Sista! Usidhani utatoka huko kwenu ukuje kutufunza kazi yetu” kijana fulani mwenye upanga mkononi alitujibu kwa ukaidi.
Angani, mawingu meusi yangeonekana yakijikusanya kama kujitayarisha kupoesha ardhi ambayo ilikuwa imechemshwa na jua kali. Ghafla, ngurumo na radi zilisikika kuashiria mvua kubwa ingenyesha wakati wotote.
“Let’s go” kiongozi wetu alitoa amri huku akituelekeza kwenye matatu ambayo ilikuwa tayari kuondoka. Hii iliashiria kilele cha matembezi yetu. Kweli! safari bado mbali kabla ya kufanikisha matarajio ya millenia.
Comments