Skip to main content

KULIFANYIKA NINI KATIKA KONGAMANO LA AFYA NA MAENDELEO - SAFARI PARK

“Aisee! nani anashukia safari park?” Makanga wa matatu ya kuelekea Githurai alipaza sauti akiuliza. “Mimi hapa!” nilimjibu huku nikikazana kupenya katikati ya abiria. Hewani, palishiba midundo mizito ya mziki iliyosambazwa kupitia spika kubwa zilizostiriwa chini ya viti.

“Hujaniregeshea change yangu!” nilimkabili makanga mlangoni. “Ulinipa pesa ngapi?” aliuliza akihema utadhani ni yeye amebeba gari kutoka mjini. Kuvutia zaidi, kijasho chembamba kilimtiririka njia mbili mbili mashavuni na kudondoka kwenye shati yake ya manjano.

Kwa sekunde chache, nilizubaishwa na mavazi ya makanga yule wa kiwiliwili cha wastani. Kichwani alivalia kofia nyekundu ya kuchujuka rangi iliyonakshiwa na maandishi “kazi kwa vijana”.Kiwiliwili kilijificha ndani ya kabuti kubwa iliyomfanya afanane "hatari bin danger"

Mashavuni palisongamana “msitu” ndevu zilizochakaa hata nikashuku ni makao wanyama pori. Taya (jaws) zake nazo zilichapa kazi ungedhani ni mtambo wa kusaga mahindi. Gololi za macho zikachomoka nje kama zitaanguka wakati wowote.

Isitoshe, alisalitiwa na alama za kijani kibichi kwenye midomo yake. Hii ilikuwa dhihirisho tosha kwamba amekopa uraibu wa mbuzi kutafuna majani. Usingoje nikufafanulie alikuwa anatafuna nini kwani hata mimi sijui. Hata labda ni sukuma wiki!

Bila kusita, alichokora mifuko ya kabuti yake kubwa kabla ya kunichomolea jani la shilingi mia moja iliyokuwa imelalia nyingine ya hamsini. “Dere funguka!....................... Dere funguka!” alimshurutisha dereva kuendelea na safari.

“Aisee! Teremka haraka tunaondoka” upesi nikaruka chini kabla ya basi kupigwa moto. Kilichobaki kuniandama ni moshi nyeusi iliyosambaa kabla ya kupaa angani. Makanga Yule alionekana akininginia kwenye mlango ya matatu kwa ustadi utadhani ni nyani imetembea jijini.

“Welcome to Safari park” kibao kikubwa kilininginia taratibu kwenye paa ya hoteli hii maarufu. Ujumbe uliotangazwa kwenye kibao hicho ilikuwa elezo tosha kwamba mazuri yalikuwa yananisubiri kule ndani. Nilitembea kwa madaha ungedhani mimi mwenyeji pale. Begi ya wastani ilitulia mgongoni, juu nilivalia sweta nyepesi ya samawati, chini jeans nyeusi nikimalizia na viatu vyeusi.

“Habari ya wakubwa?” niliamkua askari wenye sare za G4S waliokuwa wameshika doria langoni.

“Mzuri sana kaka, karibu” walipokea salamu huku wakisindikiza kwa tabasamu.
Kwa sekunde kadhaa, nilisafisha koo kabla ya kujifanya kuzungumza kizungu kwa ncha ya ulimi angalau na wajue hapo pamefika kijana maarufu. Isitoshe, nililegeza miwani na kuwatizama kiujanja. Heri tuu nisifafanue zaidi tukio hilo nitawachanganya bure!

“Excuse me guys, where is the venue of the conference dealing on health and development communication?” niliuliza na kujifanya kukohoa kidogo.
“This way please” mmoja wa askari hao alinielekeza.

Mbele yangu niliona vibao kadhaa za kusheheni nembo ya chuo kikuu cha Daystar hata nikajua nimewasili salama wasalmin. Nikichungulia kwenye kioo nyeusi, ningeona umati mkubwa wa watu uliokuwa makini kumsikiza mzee fulani aliyekuwa kasimama mbele yao kama mhubiri.

“Auuuwi! Rashidy! Hata wewe uko hapa?” kidosho aliyekuwa kwenye meza ya makaribisho aliniita kwa mashangao. Ukijipata katika hali kama hiyo utajaribu kujificha kutumia chochote kile hata ikiwa ni bakora.

“Jiandikishe hapa!” alinishurutisha huku akinisihi kushusha begi yangu.
Waume tuna ugonjwa ambao kutibu si rahisi. Ugonjwa wa kuzubaishwa na vitu vizuri na hasaa warembo. Tafadhali msishambulie kwani hata mimi nimeadhirika.

Binti huyo alibarikiwa na nywele za kipilipili, shingo ya chupa, meno meupe kama theluji yaliyo pangana kama chane kombani na kiuno cha nyigu hata akateka nyara macho pamoja na mawazo yangu nisipate kuwa makini tena.

“Ukajuaje naitwa Rashidy?” nikauliza kiujanja huku nikiwachilia macho yangu kumtalii kiumbe yule. “Kwani wadhani hujulikani, si ni wewe uliandika ile barua kwa mpenzi wako sikitu?” alinijibu kwa ujasiri.

Mashallah! Kama ningekuwa mtangazaji wa spoti ningesema nimepigwa “kumi kwa nunge”
“Tafadhali jiandikishe hapa?” alinisihi.

Singejizuia kuchungulia kitambulisho kilichokalishwa kwa lazma kwenye blausi yake kutumia kipini. Tamaa yangu kuu ikawa ni kujua jina la kiumbe huyu aliyekuwa amenichachawiza. Bana eeee! Hata wewe najua ungeadhirika. Naona aibu kusema kwamba alinifanya kusahau malengo na madhumuni ya kuzuru hoteli hiyo.

Kwa makini, nilipiga sahihi kwenye kitabu cha kuandikisha wageni kabla ya kuelekezwa katika ukumbi wa mkutano.

“Shukran kwa ukarimu wako!” nilimnongononezea kwenye sikio. “ndo wajibu wangu kaka, karibu!”alinijibu huku akitabasamu na kunivutia kiti. Tabasamu ile ilinifanya kuchanganyikiwa hata zaidi. Aligeuka na kutokomea hata nikageuza shingo na kumsindikiza kwa macho hadi alipotoka nje ya ukumbi.

Mbele ya ukumbi palisimama wima mabango ya washiriki tofauti. Macho yangu yalinata zaidi kwenye zile za chuo kikuu cha Daystar ambazo zilitangaza taaluma tofauti za kusomewa katika taasisi hiyo. Zingine zilikuwa za mashirika kama Safaricom, Internews, shirika la umoja wa kimataifa pamoja na zingine.

“Karibu katika kongamano la kujadili uandishi wa habari za afya na maendeleo 2011” kitambaa cha pamba kilichoninginia kwenye kuta kilichezeshwa na upepo uliofagilia pale ndani kila mara.

Kwa dakika chache, nilijikusanya na kusikiza kwa makini majadiliano yaliyokuwa yameshika moto. Wajumbe kutoka nchi tofauti duniani walikusanyika hapa kuwahamasisha waandishi wa habari pamoja na wadau katika sekta ya mawasiliano kukumbatia zaidi uandishi wa habari za afya na maendeleo.

Profesa mmoja maarufu mwenye mvi aliiinuka na kuwashambulia wanahabari wa nchi za kiafrika kwa kuwapa wasiasa kipaumbele na kusahau vitengo muhimu vya afya na maendeleo.

Kama kurusha mwenge penye mafuta taa, tetesi hii ilibua mabishano si kidogo haswa kutoka kwa wahariri ambao walisingizia tabia hiyo kutokana na shinikizo za wamilki wa vyombo vya habari.

Si siri, majadiliano hayo yalifana sana ila tayari nilikuwa nawasikia minyoo tumboni wakipanga kuandamana. Mara moja ama mbili nilimeza funda la mate angalau kutawanya waandamanaji hao tumboni.

“We are now breaking for lunch but we resume here for another presentation at 2PM” mmoja wa waandalizi alikatiza mkutano na kutoa tangazo hili.

usemi huo kwangu ulikuwa ni ukombozi. Hata kabla ya mshale wa saa kuteleza ukumbi uligeuka na kuwa kama soko kwani watu walitawanyika wakifuata asili ya harufu tamu ya mapochopocho.

Kwa umbali, ningezisikia glasi zikigongana hata nikajua hapa pameanguka nyota. Nje ya mlango wa kuingia ukumbi wa maankuli palisimama mabinti wawili walioshiba tabasamu. “karibuni ndani tafadhali ” mmoja wao alitusihi.

Bila kusita tulipanga foleni kabla ya kupakua chakula tofauti zilizopangwa juu ya meza ndefu. Mara nyingi nimeambiwa nistarabike na kutumia jina “buffet” badala ya kusema mengi. Haya basi ilikuwa ni buffet ya aina yake.

Kushoto kulikuwa na nyama za kila aina, sisemi mbuzi ulaya,mbuzi mtaa tafadhali endeleza orodha hii. kulia palisongamana viungo tofauti ambavo vilinichanganya kiasi ya kwamba niliogopa kusogelea huko.

Just imagine! ikiwa ningeulizwa nitambulishe kitu hapo halafu nishindwe? Bila shaka ningejifanya kigugumizi ili kujiokoa.

Keshoye, ratba ilibadilika na kuwa ya mafunzo kwa wanahabari. Usishangae nilimisi hata mandhari ya hoteli kwani kikao chetu kilihamishwa hadi kitovu cha jiji la Nairobi katika afisi za Internews kwenye orofa ya I&M.

Huko, nilipata kugundua kwamba wanahabari wengi huogopea sana takwimu kama mauti. Mafundisho haya yalitekelezwa na wanahabari wa kimataifa ambao ni mabingwa katika fani mbalimbali za uanahabari.

Wa kunivutia sana, ni mhariri mkuu wa gazeti la “The people daily.” kisa na maana, alitufafanulia kwa kina mbivu na mbichi kuhusu habari za upekuzi. Nikimnukuu, alisema fani hiyo si ya wengi na kwa wale wachache wenye kufanisi katika fani hiyo wamepewa heshima si kidogo.

Isitoshe, alisimulia kuhusu wanahabari kadhaa waliohatarisha maisha yao ili kuanika hadharani sakata za serikali kuwafilisi walipa kodi. Mmoja aliyenisikitisha sana ni marehemu Bw.Munuhe aliyewawa kwa kutishia kutangaza maficho ya Bw.Felicien Kabuga anayetuhumiwa kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda.

Tosha gari, tuelekee katika siku ya tatu. Kikao kilifunguliwa na na viumbe wazito katika anga za mawasiliano nchini. Mmoja kama huyo ni Bw.Ezekiel Mutua wa wizara ya habari na mawasiliano. Bila kupima maneno aliwakemea wanahabari ambao wameegemea sana upande wa siasa na kufungia jicho habari zinazohusu afya na maendeleo kwa kisingizio kwangu watu hawazipendi.

Isitoshe mandugu zetu kutoka Nigeria waliwakilishwa na wataalamu kutoka vyuo vikuu tofauti za ulaya. Kama kawaida yao usemi wao uliambukizwa vitendawili na misemo ambayo iliwacha wengi wakilia mbavu.

Kama ada, kikao kilivunjwa mara kwa mara na kiburudisho cha vinywaji pamoja na vinyamunyamu tofauti.
Endelea kufuata hadithi hii wiki ijayo………………………………………..

Comments

kipande cha pili kiko jikoni: mniwie radhi kwa kuchelewa kwake ni shida tuu za kimitambo

Popular posts from this blog

MAZINGAOMBWE YA SAA

Na Danyell Odhiambo Nimejirusha kwenye kiti kilegevu cha msonobari nikifikiria jinsi hali ya maisha nchini Kenya inavyozidi kupaa kila uchao. Mbele yangu, pametulia redio, kando pamesimama kikombe cha kahawa chungu na juu pananinginia saa ya ukuta. Ghafla, fikra zangu zinatekwa nyara na saa iliyozubaa ukutani. Nikiangazaangaza, naona imetimia usiku mkuu. Hii ni kumaanisha, mishale yote ya saa imekutana kifuani pa namba kumi na mbili. Ukipiga hesabu kwa makini, utakubalina nami kwamba tukio kama hili hujirudia mara mia tatu sitini na tano kila mwaka. Ukumbuke, kisa hiki pia huashiria kuzaliwa kwa siku mpya. Hata ingawa mishale hizi zimedhibitisha ushirikiano ni kiungo muhimu katika katika kikundi, taswira fulani inaibuka nikiangalia mishale hizo. Taswira yenyewe yahusu tabia mbovu ya wabunge kukaidi shinikizo za kuwataka kulipa malimbikizi yao ya kodi. Nikipamabanua kitendawili hiki, itakubali kwamba jamii imejigawanya kupitia mishale hizi tatu za saa. Mahuluku taabu nawafa...

MAPENZI KIZUNGU ZUNGU

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL Mawimbi makali baharini yalikimbizana na hatimaye kusukuma maji hadi ufukweni. Pembeni, Bahati alionekana ameshika kijiti kirefu mkononi akijaribu kuchora umbo la moyo wa mapenzi kwenye changarawe mbichi huku maji ya bahari yakifuta. Angani, ndege aina ya korongo na mbayu wayu wangeonekana wakicheza cheza huku tufani kali zikifanya matawi ya minazi ufuoni kupukutika. Nikijistiri juu ya roshani(balcony) katika hoteli ambayo tulikuwa tumekodisha nilisalia kula kwa macho. Nilibakia kinywa wazi kuona madhari ya kutamanisha jinsi jua ilizama upeoni na kufanya maji ya bahari kupiga rangi ya manjano. mawazoni, nilitawaliwa na picha za harusi yetu jana yake katika ukumbi wa pataneni . Hatua chache niliona suti yangu ambayo ilikuwa ingali sakafuni baada ya usiku yenye sarakasi si kidogo. Ajabu, marashi yenye uhai aliyopiga Bahati ilikuwa bado imesakama pua yangu.Waliosema harusi ni kilele cha mapenzi hawakukosea hata kidogo. “Honey…………Rashidy! Rashidy!” Kwa...

SIRI ZA “JAM” JIJINI NAIROBI; TOLEO LA PILI

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL Jinsi basi lilivyozidi kufukuzia kuelekea mzunguko wa Nyayo stadium, ndivyo ilizidi kuwachilia moshi ya mpingo iliyosokota angani kabla ya kutawanyika. Pale pia, tulimpata polisi wa trafiki mwanamke aliyefungia mshipi wa longi yake kwenye kifua. Amini usiamini, kwa ishara ya mkono alielekeza mkondo wa gari kama jinsi upepo huele ... keza bendera. Pale tulis...imama kwa dakika chache kabla ya msongamano kufunguliwa. Cha kuvutia tamaa ya macho yangu ilikuwa ‘tuk tuk’ fulani ambayo ilipenya penya kati kati ya magari huku ikipiga kelele kama mashine ya kusaga mahindi. Wenzangu wanaiita kule bara POSHOMILL. “We! Boss, ondoa hiyo kabati kwenye barabara” alisikika akishambuliwa na mmoja wa madereva wa matatu. Wanasema muungwana hununa moyoni na wala siyo mashavuni na kwa hivyo Yule dereva wa ‘tuk tuk’ akaridhia kumjibu kwa kimya. Kando na tukio hili, kuna jambo lililotendeka ambalo liliwacha mbavu za kila mtu zikiuma. Niseme nisiseme! Aaaah! ...