Skip to main content

KIVULI KIZITO CHA KIWEWE



MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL

Wa kwanza alikuwa Rehema, njia zetu zilikutana kwenye ufuo wa bahari hindi msimu wa upanzi wa mwaka 1999. Kidonda hicho kingali kibichi. Japo nilibaki na kovu, nahisi ni kama nazungumzia ya jana. Kwa ufupi, yake na yangu yalikuwa mafupi hata ingawa vioja vilikuwa teletele. Uhusiano wa kunoga tulilinda kwa takriban miezi miwili.


Siku moja, aliamka na kuniambia yu mja mzito. Nilimshauri akakiangamize kijusi hicho. Hii ilitokana na wingi wa uoga kuhusu majukumu ambayo yangendamana na hali hiyo. Alikubali wito japo shingo upande. Baadaye, niliarifiwa yuko hali mahututi katika katika zahanati ya Dr. Tiba wa Maradhi. Kesho yake Jioni , nilipata simu ya dharura. “harakisha mpenzio amevuja damu nyingi sana akijaribu kuavya mimba changa. Nasikitika kusema, si wa dunia hii tena.” hitimisho likawa ni maombolezi na baadaye mazishi huku vidole zote nikielekezewa.

Vivyo hivyo, aliyefuatilia mkondo huu alikuwa kipusa kwa jina Amina. Mtoto yatima ambaye nilipata kumjua kupitia rafiki yangu aliyekuwa afisa wa umma katika makao ya watoto ya Huruma. Nilimlisha, nikamvisha na hata kumpa penzi ambalo nilijua kilele ingekuwa ni harusi. Lakini, kama wasemavyo. binadamu hupanga, mungu naye akapangua. Mpenzi wangu alifariki dunia katika ajali mbaya kwenye barabara ya kuelekea mji wa salama.


Wa tatu naye alikuwa ‘black beauty’ almaarufu cheusi chan’gaa kwa jina Anyango. Huyu naye alikuwa msichana wa chuo kikuu. Taaluma yake ilikuwa udakitari. Tulikutana katika tamasha la kusheherekea utamaduni katika ukumbi wa Pataneni. Hapa nilidhani nimegonga ndipo kwa vile ishara zote zilionesha bibi nilikuwa nishamtia kiganjani. Nilimrai akubali azma yangu ya kumvisha pete lakini aliabudu zaidi anasa. Tulimzika yapita miaka mitatu baada yake kunywa sumu alipogundua ameambukizwa virusi vya ukimwi.


Jaribio langu la nne lilikwa ni dada kwa jina Chebet, mtangazaji maarufu wa televisheni na pia mwanariadha shupavu. Amini usiamini, raundi hii nilijua pamehusika kudra ya maulana. Sawa na hapo awali, penzi liliota kwenye mchanga wenye rutuba. Kadri siku zilivyo shikana na kuwa miezi ndivyo huba ilinawiri na kuganda.


Kitumbua kiliingia mchanga jioni moja aliponifumania nikifanya masihara na kijakazi mmoja pale kijijini. Heri nilitaje kama masihara. Kwa vile, nikifafanua zaidi nitaona aibu kiasi ya kwamba nitakosa hamu ya kuendelea na waraka huu. Cha mno ni kwamba, siku moja baada ya tukio hilo, niligutushwa na kamsa aliyepata mwili wake ukininginia kwenye mbuyu mkongwe kijijini.


Hatari zaidi, aliwacha waraka fupi kueleza sababu ya kauli hiyo iliyowacha kila mtu kinywa wazi. Kwa mara nyingine, vidole nilinyoshewa huku nikigeuzwa chombo cha kupigiwa mfano katika ushauri wowote kuhusu usherati. Hata hivyo, wanasema mchumia janga hula na wakwao. Kwa hivyo ilinibidi kufukuzwa kijijini baada ya kuzuka tuhuma kwamba nilikuwa nimewapaka wanakijiji aibu.


Hiyo ilikuwa ni miaka miwili kabla ya kukubaliwa kurudi nyumbani mwezi jana. Leo, nimekutana na dada Sikitu. Si mahala pengine ila ni katika jumba la ibada. Kwa umbali, natambua ana baadhi ya sifa za kimaumbile walizokuwa nazo Rehema, Amina, Chebet na hata dada Anyango. Natamani kupata muda wa kutoa malilio ya moyo wangu ila naogopa kumjumlisha katika msururu wa mkosi ambao umetawala maisha yangu.


Sitaki ajue kwamba wiki nyingi ambazo zimepita nimekuwa nikipokea matibabu kutoka kwa mganga mmoja maarufu nchini jirani ili kutibua balaa zinazonifuata. Si siri, waganga nimefukuzia kusini, kaskazi, kushoto hata kulia bila mafanikio. Niliona safari hizi ni hasara tupu ndiposa nikajishauri kufuata njia ya kidini angalau nishushiwe mzigo huu.


Hata ingawa tambiko zimefanywa na magoti kupigwa ili kunikomboa, ningali nimetekwa nyara na uoga kwamba marudio ya balaa yangali yananikodolea macho. Kutoka mahala nilipoketi nyuma ya kanisa, nawaona wanadada wa kila aina. Wembamba, wanono, warefu, wafupi, weusi na hata weupe lakini gundi la huba limenielekeza kwake Sikitu.

Sina tofauti na bubu ambaye anahisi njaa ila hawezi kuagiza chakula. Sina tofauti na kipofu ambaye amewekwa kwenye mwangaza ila hawezi kujielekeza. Ni kitendawili ambacho kimepooza ulimi wangu nisijue la kusema.

Kwa makini nilifuatilia ibada huku nikisawiri biblia kudaka sehemu alizonukuu askofu. Kwa dakika kadhaa, nilitembeza macho huku na kule nikajipata nimerudi alipoketi mpenzi mtarajiwa.

Muda huu wote nilikuwa nimejikunyata mithili ya kuku aliyenyeshewa. Kando yangu alikuwa jibabu moja la kutiririkwa jasho njia mbili mbili mashavuni. Hii ni kutokana na wimbi la joto lililofagilia kanisani. Babu alishika kitambaa chake na kupangusa jasho toka kilele cha kipara utosini hadi kwenye videvu vya kuchakaa kama beberu.

Ajabu ni kwamba, kinyume na hali ya kawaida mwili uliganda utadhani nimedungwa sindano ya barafu. Ikulu ya baridi ikawa ni moyo wangu mlegevu ambao ulibadikia na kuwa bohari ya kuhifadhi magunia ya upweke. Wakati mmoja nilizubaa nikimwangalia sikitu hadi akanishika ‘red handed’. Lililobaki lika
wa ni kubadilishana tabasamu huku ……..tuendelee ama tusiendeleee?

Comments

Popular posts from this blog

MAZINGAOMBWE YA SAA

Na Danyell Odhiambo Nimejirusha kwenye kiti kilegevu cha msonobari nikifikiria jinsi hali ya maisha nchini Kenya inavyozidi kupaa kila uchao. Mbele yangu, pametulia redio, kando pamesimama kikombe cha kahawa chungu na juu pananinginia saa ya ukuta. Ghafla, fikra zangu zinatekwa nyara na saa iliyozubaa ukutani. Nikiangazaangaza, naona imetimia usiku mkuu. Hii ni kumaanisha, mishale yote ya saa imekutana kifuani pa namba kumi na mbili. Ukipiga hesabu kwa makini, utakubalina nami kwamba tukio kama hili hujirudia mara mia tatu sitini na tano kila mwaka. Ukumbuke, kisa hiki pia huashiria kuzaliwa kwa siku mpya. Hata ingawa mishale hizi zimedhibitisha ushirikiano ni kiungo muhimu katika katika kikundi, taswira fulani inaibuka nikiangalia mishale hizo. Taswira yenyewe yahusu tabia mbovu ya wabunge kukaidi shinikizo za kuwataka kulipa malimbikizi yao ya kodi. Nikipamabanua kitendawili hiki, itakubali kwamba jamii imejigawanya kupitia mishale hizi tatu za saa. Mahuluku taabu nawafa...

MAPENZI KIZUNGU ZUNGU

MTUNZI: ODHIAMBO DANYELL Mawimbi makali baharini yalikimbizana na hatimaye kusukuma maji hadi ufukweni. Pembeni, Bahati alionekana ameshika kijiti kirefu mkononi akijaribu kuchora umbo la moyo wa mapenzi kwenye changarawe mbichi huku maji ya bahari yakifuta. Angani, ndege aina ya korongo na mbayu wayu wangeonekana wakicheza cheza huku tufani kali zikifanya matawi ya minazi ufuoni kupukutika. Nikijistiri juu ya roshani(balcony) katika hoteli ambayo tulikuwa tumekodisha nilisalia kula kwa macho. Nilibakia kinywa wazi kuona madhari ya kutamanisha jinsi jua ilizama upeoni na kufanya maji ya bahari kupiga rangi ya manjano. mawazoni, nilitawaliwa na picha za harusi yetu jana yake katika ukumbi wa pataneni . Hatua chache niliona suti yangu ambayo ilikuwa ingali sakafuni baada ya usiku yenye sarakasi si kidogo. Ajabu, marashi yenye uhai aliyopiga Bahati ilikuwa bado imesakama pua yangu.Waliosema harusi ni kilele cha mapenzi hawakukosea hata kidogo. “Honey…………Rashidy! Rashidy!” Kwa...

SIRI ZA CHUO KIKUU CHA DAYSTAR

Njoo unisome kwa makini S.L.P 927 MACHO PLAZA Kwa wewe unayenisoma, Habari za utokako? Naona unahema kweli ukitaka kujua yaliyojiri hivi leo kwenye barua hii. Hee! By the way, ikiwa wataka tuelewane naomba uwache kuniangalia kwa hizo macho za kushiba chuki na dharau. Kabla nikuendelezee udaku! Tafadhali wacha kuangalia kando kando ukinisoma. Unawafanya wapita njia wanadhani tunawasengenya humu. By the way, usha ambiwa na yeyote hivi leo kwamba watamanisha? Ooooooooooooh! Nisamehe. I mean.... you are fearfully and wonderfully made. Sitaongeza wala sitapunguza. Niwie radhi siwes kutranslate, please! Mwelezee.. aliye kando yako aje akusaidie. Kabla nikupatie udaku, natamani niulize swali moja tuu. Nihakikishie kwamba hutanuna! Naogopa lakini heri niulize tuu atleast tusafiane nia. Hivi mbona una blush sana? Kama nimekubamba si uniambie tuu ama uwaite wanafunzi wenzako waje wasome uhondo. Matawi ya miti naona inapukutika kutokana na upepo mkali unaofagilia kutoka milima ya l...